Zilizopendwa Zaidi

Wapendwa
Breaking
Inapakia...

JIONEE HISTORIA YA BBC SWAHILI TANGU 1959 ILIYOANZISHWA NA OSCAR KAMBONA

Historia ya Idhaa ya Kiswahili

Salim Kikeke kazini uchaguzi wa Tanzania 2010  

''Hii ni London. Leo kwa mara ya kwanza kabisa BBC inawapa salamu wakazi wa Afrika mashariki kwa lugha yao. Asalaam Aleikum,"sauti tulivu ya Oscar Kambona ilisikika hewani miaka 60 iliyopita.
Idhaa mpya ikawa imezaliwa - Idhaa ya Kiswahili ya BBC.
Kambona alikuwa mwanafunzi kutoka Tanzania aliyekuwa akisomea Uingereza.
'Mtoto' huyo aliyezaliwa miongo sita iliyopita aliibuka na kuwa idhaa ambayo imekuwa ikiaminika sana miongoni mwa mamilioni ya wasikilizaji Afrika Mashariki na Kati na mataifa ya ughaibuni. Hata sasa, licha ya 'umri wake' sauti yake haijashika kutu au kudhoofika, imani ipo pale pale.
Mwaka 1957, mwezi Machi, kulishuhudiwa mabadiliko makubwa ya kisiasa katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara. Ghana ikawa nchi ya kwanza kujipatia uhuru na kutoa mwelekeo kwa nchi nyingine za eneo hilo.
Tangu kuzinduliwa tarehe 27 mwezi Juni mwaka 1957, Idhaa ya kiswahili ya BBC, ilitangaza habari kuhusu vita vya kujitafutia uhuru na pia sherehe za baada ya kujipatia uhuru Tanganyika, Uganda, Kenya, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda na Burundi.
Idhaa ya Kiswahili ya BBC iliwapa fursa waasisi wan chi hizo kama vile Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta na Milton Obote wa Uganda fursa ya kuendeleza itikadi zao.
Idhaa hii ilijipatia sifa ya ujasiri kwa jinsi ilivyotangaza uvamizi wa Tanzania nchini Uganda ili kumaliza utawala wa kiimla wa Idi Amin mwaka 1972 na pia hatua ya Rwanda na Uganda kutimua dikteta mwingine Mobutu Sese Seko wa Zaire ambayo sasa inajulikana kama Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliyeondolewa mamlakani 1997.
Abdulaziz Yacoub
Mtangazaji wa BBC Swahili Abdulaziz Yacoub alikijionea gari aina ya Rolls Royce Silver Cloud wakati wa maonesho ya magari ya Motor Show jijini London mwaka 1958
Kwa miaka mingi Idhaa ya Kiswahili ya BBC ilitawala masafa ya utangazaji Afrika Mashariki na kati kwani ilikuwa njia mbadala ya kupata habari kwa vyombo vilivyomilikiwa na serikali.
Na huku idhaa ya Kiswahili ya BBC ikitimiza miaka 60, inakabiliwa na changamoto nyingi. Ushindani sana kutoka stesheni za masafa ya FM.
Kinyume na zamani, vituo vya kibinafsi vimeongezeka sana.
Isitoshe, teknolojia imebadilika na siku hizi watu wanajipatia habari, taarifa na burudani kupitia tovuti na mitandao ya kijamii.
Mahitaji ya wasikilizaji pia yamebadilika pakubwa kutokana na uhamasisho na kuongezeka kwa njia za kujipatia habari.
 Salim Kikeke kazini
Salim Kikeke kazini wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2010
Siku hizi, kinyume na zamani, taarifa kuhusu kutokea kwa jambo huenea haraka na wasikilizaji huwa hawalazimiki kusubiri hadi mshale wa saa ugonge, ndipo wafahamu yaliyojiri pande mbalimbali za dunia.
Kari Blackburn ambaye alikuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC mwaka 1996 hadi 1999 anakumbuka baadhi ya matukio muhimu wakati huo.
''Ulikuwa wakati wa mabadiliko makubwa kwa utanagazaji wa radio Afrika Mashariki na tulifahamu tosha kuwa hata mashabiki wetu hawangevumilia matangazo ya masafa mafupi baada ya kusikiliza matangazo ya FM ambayo yalisikika vizuri zaidi.''
Emmanuel Vivian Kassembe
Emmanuel Vivian Kassembe wa BBC Swahili mwaka 1964
Kwahivyo pamoja na Barry Langridge, Michel Lobelle na Tido Mhando tukaanzisha ushirikiano na vyombo vikubwa vya habari nchini Tanzania kama IPP na Radio Free Africa.
''Wakati wa maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Idhaa ya Kiswahili ya BBC aliyekuwa Rais wakati huo Daniel arap Moi akatupa idhini ya kutangaza kwa vipimo vya FM Nairobi na Mombasa."
''Wakati huo tulifanya mabadiliko makubwa katika vipindi vyetu na kuvipa majina kwa mara ya kwanza-Amka na BBC," Dira ya Dunia na Leo Afrika.''
''Kama mwanamke wa kwanza kuongoza Idhaa hii nilijitahidi sana kuwavutia wanahabari mashuhuri wa kike kama Mariam Omar, Suzanne Mungy na Vicky Ntetema."
Mrithi wa Kari Blackburn, Tido Mhando alikuwa mwenye bidii ya aina yake.
Tido Mhando alifanya mahojiano na marias wengi. Daniel arap Moi wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda, aliyekuwa Rais wa Tanzanian Benjamin Mkapa na mrithi wake Jakaya Kikwete, Paul Kagame wa Rwanda, aliyekuwa Rais wa Msumbiji Joachim Chissano na Joseph Kabila wa DRC ambaye alimrithi babake Laurent Kabila.
Tido alikuwa mwandishi wa habari wa mwisho kumhoji Laurent Kabila siku chache kabla ya kuuawa kwake mwaka 2001.
''Kwa kuwa marais wengi walikubali tuwahoji ni hiyo ilikuwa ishara kwamba waliiamini BBC,'' anasema.
''Tulipata mafanikio makubwa. Tulifungua ofisi katika eneo letu na tukahakikisha waandishi wetu wamepata vifaa vya kufanya kazi''.
''Idhaa ya Kiswahili ya BBC ilikuwa idhaa ya kwanza ambayo sio ya kiingereza kutangaza Ligi ya Premia ya Uingereza kwa wasikilizaji wa Kiswahili.''
''Huenda hatua kubwa tuliyopiga ni kuhamisha matangazo yetu ya asubuhi, Amka na BBC kutoka London hadi Nairobi. Tulitaka kuwa karibu na wasikilizaji wetu.''
 Angela Ng'endo na Beth Mugo
Angela Ng'endo akimhoji aliyekuwa waziri wa afya Kenya Beth Mugo mwaka 2012
Matangazo hayo ya Amka na BBC baadaye yalihamishiwa jijini Dar es Salaam.
Kwa Tido, maisha katika Idhaa ya Kiswahili ya BBC yalikuwa ya kuchangamsha. ''Kila mwaka tulikuwa tukishugulikia mambo mapya. Tulitaka kutimiza mahitaji ya wasikilizaji.''
Kwa sasa idadi ya wasikilizaji, wasomaji na watazamaji wa Idhaa ya Kiswahi ya BBC imefikia 16 milioni.
 Odhiambo Joseph
Odhiambo Joseph akizungumza na dadake Marehemu Idi Amin, Dee Amin mwaka 2011
Mhariri wa sasa wa BBC Swahili Caroline Karobia anasema, "Tunajivunia sana historia yetu ya utangazaji na tunatumai kwamba tutaweza kuendelea kuimarika na kuwahudumia wasikilizaji na watazamaji wetu wka miaka mingi ijayo. Tuna furaha sana kutokana na fursa zinazoletwa na teknolojia mpya kutuwezesha kufikia watu wengi zaidi na kwa karibu zaidi."


Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 maoni :

Chapisha Maoni