Tahadhari:
Makala hii ina maelezo, Picha na Video ambazo zinaweza kuwa za kuogofya
au kuchefua kwa baadhi ya watu. Tafadhali soma kwa tahadhari binafsi.
Pia si lengo la makala hii kupinga au kokosoa imani ya mtu yeyote. Hivyo
basi epuka kutoa maoni yanayoweza kuleta hisia za kukinzana au kukwaza
imani za wengine.
Nashukuru kwa kunielewa!
Mchinjaji Muhammad al-Beshi
Al-Beshi akiwaonyesha waandishi wa Habari jambia lake analotumia kuchinijia, alupofanta mahojiano na Arab News mwaka 2003
Deera Square, Riyadh (Saudi Arabia)
Ni takribani saa mbili na nusu asubuhi katika eneo la wazi la Deera
Square lililopo kwenye mji wa Riyadh katikati ya nchi ya Saudi Arabia.
Polisi maalumu wa kitengo cha Mutaween wanawatawanya watu waliopo
eneo hilo ambao wengine wamepumzika tu na wengine wapita njia. Polisi
hawa ni maalumu wanatambulika kisheria chini ya muongozo wa Shari'ah (kanuni za Kiislamu) ambayo ndiyo kwa kiwango kikubwa inatumika kuongoza taifa la Saudi Arabia, kazi kuu ya askari hawa maalumu ni kuhahakisha kuwa Sharia ya Kiislamu (kwa mujibu wa wao Saudi Arabia walivyo tafsiri) inafuatwa nchini humo.
Mutaween wanahakikisha kuwa wananchi wanafuata utaratibu wa vitu kama
mavazi ya heshima (kwa mujibu wa Sharia), kutouzwa vileo mitaani,
kutouzwa vyakula 'haramu' kama vile nyama ya nguruwe, vijana
kutosikiliza nyimbo za kimagharibi au filamu, pia kuhakikisha wanawake
'wanajisitiri' na hawaongozani na wanaume ambao si waume zao au ndugu
zao. Askari hawa ambao sare zao ni kanzu pamoja na viremba maridhawa vya
kiarabu wanazunguka mitaani kila kukicha kuhakikisha kuwa Sharia inafuatwa.
Leo hii wapo hapa eneo la Deera Square wakiwaondoa watu kwenye eneo
hili, ili kupisha tukio maalumu ambalo linatarajiwa kufanyika mahali
hapa.
Eneo hili la Deera Square ukubwa wake bado kidogo lingeweza kufanana na ukubwa wa kiwanja cha mpira. Upande wa
kulia wa uwanja huu kuna msikiti mkubwa sana maarufu ambao watu wengi
husali hapo, na upande wa kushoto kuna majengo ya ofisi za askari hawa
wa Mutaween.
Majengo yanayozunguka uwanja huu wa Deera Square yote yana kuta
maridhawa za rangi ya njano zinazofanya muda wa mchana jua kali likipiga
eneo hili kujiakisi kwa rangi fulani kama ya dhahabu ambayo haijapita
kwenye moto.
Pia kwenye kingo za uwanja kumepandwa michikichi mirefu ya wastani na imepandwa kwa ustadi kwenye mishari kwa
kupendeza kabisa. Na si hivyo tu, eneo hili karibu na msikiti upande wa
kulia kuna chemi chemi ya urembo ya maji (water fountain) ambayo
inarusha maji hewani kwa madaha na kuleta msisimuko wa kupendeza katika
eneo hili la uwanja huu tupu mkubwa.
Kwa mtu mgeni unaweza kujihoji eneo hili kubwa namna hii lina matumizi
gani hasa? Uwanja ni mkubwa mno kutaka kukaribia uwanja wa mpira wa
miguu, lakini hakuna shughuli zozote zinazoendelea zaidi ya wapita njia
tu.
Vitu pekee vinavyoonekana kwenye uwanja huu mkubwa ni kama nilivyoeleza,
michikichi iliyopandwa kwa ustadi, 'water fountain' na msitikiti upande
wa kulia na ofisi za Mutaween upande wa kushoto.
Muda huu wa saa mbili na nusu asubuhi kama nilivyoeleza, askari walikuwa
wanajaribu kuwaondoa watu waliokaa eneo hili au wale wanaopita njia.
Lengo lao ni uwanja huu ubaki mtupu. Lakini ajabu ni kwamba kadiri
askari wanavyojaribu kuondoa watu kwenye eneo hili, ndivyo ambavyo watu
wengine wengi zaidi wanazidi kumiminika mahala hapa wakiwa na shauku na morari kana kwamba wanaenda kushangilia timu yao pendwa ya mpira wa miguu.
Deera Square, Riyadh
Watu wakiwa wamefurika Deera Square Kushuhudia tukio muhimu la Hukumu
Kutokana na watu kuzidi kumiminika eneo hili baada ya askari kuanza
kuwatawanya ni dhahiri kwamba hii inaonyesha kuwa hii si mara ya kwanza
na hii ni desturi, kwahiyo walikuwa wanajua fika ni nini kilikuwa
kinaelekea kutokea mahali hapa.
Hii inawafanya maaskari waweke uzio wa kamba maalumu ya eneo la tukio
('police' scene tape) ili kuzuia umati wa watu usiweze kusogea mpaka
eneo la katikati la uwanja huu.
Kama ni mgeni unaweza kujikuta unavutika kusogea mahali hapa ili uweze kujua ni kitu gani hiki cha kusisimua lilikuwa linajiri.
Lakini matumaini yako ya tukio la kusisimua yataanza kuyeyuka ghafla
mara baada ya kuona magari yapatayo matatu ya Polisi aina ya jeep
yakiwasili mahala hapo na polisi kuanza kushuka.
Kwa kawaida ghafla umati wote uliokusanyika hapo unakuwa kimya baada ya
kuona magari haya ya polisi. Ukimya unaogubika ghafla umati huu ni
mkubwa kiasi kwamba unaweza kujikuta unatokwa jasho la presha kupanda
kutokana na kutokujua ni nini kilikuwa kinafuata. Hakuna mtu
anayethubutu hata kutingishika au kukohoa, wote wanakodolea macho tu
magari haya matatu ya polisi yaliyowasili.
Ukimya na uoga unaotawala nyuso za watazamaji hawa waliojikusanya unaweza kuhoji ni kwanini wefika mahali hapa kuja kushuhudia jambo hili linalotaka kufanyika.
Katika ukimya huu huu mkubwa, wanashuka mapolisi si chini ya kumi na
mbili waliovalia sare, sita kutoka gari la mbele na sita kutoka gari la
nyuma. Wakishashuka kila mmoja anaenda kujipanga katika eneo lake
kuzunguka eneo lote la katikati ya uwanja.
Katika hatua hii ukimya unaongezeka zaidi kiasi kwamba kama ikitokea
labda mtu amedondosha sarafu mita ishirini na uliposimama wewe unaweza
kujikuta unasikia. Ukimya unakuwa mkubwa zaidi kiasi cha kuogofya, na
kinachoweza kukutisha zaidi ni nyuso za morari za watazamaji hawa waliozunguka uwanja huu wa Deera Square.
Baada ya hapo lile gari moja lililosalia (gari la kati kati) milango
inafunguliwa, na kisha wanashuka maaskari wanne ambao nao wanakuwa
wamevalia sare za kipolisi, lakini tofauti na maaskari wale kumi na
mbili walioshuka mwanzoni, hawa wao wanashuka kwenye gari wakiwa
wameongozana na mtu mwingine wa tano ambaye yeye hajavalia kipolisi.
Mtu huyu anakuwa amevikwa mavazi meupe sana, au kama wasemavyo watu, "mavazi meupe peeeee"! Yaani weupe ambao unaweza kuumiza macho jua kali linapoakisi. Lakini mtu huyu anakuwa amefungwa mikono yake kwa kamba kwa nyuma na usoni anakuwa amefungwa kitambaa cheusi.
Maaskari wawili kati ya wale wanne walioshuka kwenye gari, wanamshika
mtu huyu na kumuongoza mpaka kati kati ya uwanja na wakiisha kumfikisha
katikati ya uwanja jambo la kwanza wanalolifanya ni kumpigisha magoti.
Mara chache baada ya kumpigisha magoti wanaweza kumfunika na fuko la kitambaa jeusi usoni (licha ya kuwa tayari
amefungwa litambaa cheusi machoni) lakini mara nyingi wanaweza kumuacha
hivyo na kitambaa cheusi tu machoni mara baada ya kumpigisha magoti.
Mpaka kufikia hatua hii mtu huyu aliyepigishwa magoti anakuwa tayari kwa ajili ya kuchinjwa.!!
Na ghafla tu utasikia sauti kwenye spika zilizofungwa kwenye pembe za
uwanja huu, zikitangaza kosa la mtu huyo na hukumu yake kwa mujibu wa
Sharia.
Kisha askari mmoja anamfuata huyu mtu aliyepigishwa magoti na
kumuinamisha shingo yake kuelekea mbele, kumuandaa kwa ajili ya
mchunjajia maalumu wa serikali kupitisha upanga shingoni mwake.
Kisha umati wote unaoshuhudia, pamoja na polisi… wote kwa pamoja
wanabakia kumsubiri mtu maalumu wa kutekeleza shughuli hiyo, mtu ambaye
labda ndiye aliyechinja zaidi binadamu wenzake wengi kwenye historia ya
dunia kuliko mtu yeyote… umati wote, wakiwa kwenye ukimya huu mkuu, na
hofu iliyochanganyika na morali wanamsubiria Muhammad Saad al-Beshi.
SIKU MOJA KABLA
Siku moja kabla ya raia aliyehukumiwa kifo nchini Saudi Arabia kuchinjwa hadharani, kwanza mchinjaji Muhammad Saad
al-Beshi hutembelea familia ya muhusika ili kuomba msamaha. Msamaha huu
anaomba al-Beshi si kwa ajili yake bali anaomba kwa ajili ya mtu
anayeenda kumchinja kesho yake ili ndugu zake wapate kumsamehe aondoke
duniani akiwa hana lawama kutoka kwa jamaa zake.
Moja ya swali ambalo binafsi niliwahi kujiuliza au yawezekana pia nawe
uko unajiuliza muda huu, ni namna gani al-Beshi alifikia hatua ya kuwa
"mchinjaji rasmi" wa serikali ya Saudi Arabia? Kuna sifa gani hasa
zinaangaliwa? Al-Beshi anajisikiaje kuondoa uhai wa binadamu mwingine kikatilli namna hii?
Katika mahojiano ya nadra sana ambayo aliyafana na Arab News mwaka 2003
al-Beshi aliwahi kueleza ni namna gani alijikuta anaingia katika ajira
hii ya "kipekee".
Al-Beshi alianza kazi ya kuchinja watu mwaka 1998, kabla ya hapo alikuwa anafanya kazi gerezani maeneo ya Taif, na kazi yake ili kuwa kuwafunga mikono na vitambaa vyeusi machoni wafungwa ambao walikuwa wanapelekwa kuchinjwa.
Baada ya muda akajikuta anaanza kutamani na yeye 'kupanda cheo' ili awe mchinjaji.
Ikatokea kuna muda serikali ikatangaza nafasi ya kazi kwa ajili ya mchinjaji na hila kusita akaomba nafasi hiyo na kukubaliwa.
Mara yake ya kwanza kuchinja mtu ilikuwa ni mwaka 1998. Al-Beshi
anaeleza kuwa siku hiyo alikuwa na hofu sana na hasa kutokana na umati
wa watu uliojitokeza.
Beshi anasema kuwa alipofika eneo la kuchinjia, alimuinamisha mtuhumiwa
shingo na kumpiga upanga mara moja shingoni kwa kishindo kikubwa na
kumtenganisha kichwa na kiwili wili.
Siku yake hii ya kwanza kuchinja mtu, Beshi anadai kuwa hakupata
usingizi usiku, lakini baada ya hapo hajawahi tena kuwa na hofu wala
kukosa usingizi.
Mpaka sasa ameshachinja mamia ya binadamu kwa ruhusa ya serikali ya
Saudi Arabia na inaelezwa kuwa yeye ndiye anayeongoza kwa kuchinjwa watu
wengi na ndiye mchinjaji chaguo la kwanza la serikali pale
inapohitajika mtu kuchinjwa hadharani baada ya kuhukumiwa.
Beshi anaeleza kuwa kuna kipindi huwa anachinja mpaka watu kumi kwa siku moja.
Al-Beshi anajitetea kuwa yeye si mtu katili kwa sababu ya kazi
anayoifanya, kwani anajisikia fahari kufanya kazi hiyo ya mchinjaji kwa
kuwa anaamini anafanya kazi ya mwenyezi Mungu kama ilivyoagizwa kwenye
vitabu.
Pia anaendelea kujitetea kwamba kazi yake haimtengi na jamii kwa kuwa
ana marafiki wengi msikitini na mtaaani, pia ana ndugu na jamaa ambao
wanampenda na kumuelewa juu ya chaguzi yake hiyo ya ajira.
Si hivyo tu, bali pia al-Beshi ni mume ameoa na amejaaliwa kupata watoto saba.
Al-Beshi anaeleza kuwa huwa anawaruhusu watoto wake kumsaidia kusafisha
damu sime lake pindi akitoka kazini kwenye kuchinja watu Deera Square.
Moja ya watoto wake anayeitwa Musaed ambaye ana miaka 22, ameanza
'kumtrain' ili aje kufanya kazi hiyo ya uchinjaji miaka ya baadae.
Siku ya kwanza baada ya kukabidhiwa jukumu hili la kuwa mchinjaji wa serikali, al-Beshi alikabidhiwa sime maalumu na serikali kwa ajili ya kutekeleza jukumu hili.
Sime hili linaelezwa kuwa na thamani ya Riyal 20,000 za Saudi Arabia (zaidi ya dola 6,000 za marekani).
Al-Beshi anaeleza kuwa sime hili ni moja kati ya vitu muhimu zaidi kwenye maisha yake anavyovitunza kwa uangalifu
mkubwa sana kwa kuwa sime anaona ni kama heshima kubwa kwake aliyopewa
na serikali ya Saudi Arabia ili aweze kufanya kazi ya Mungu.
Beshi haishii hapo tu, bali pia anaeleza namna watuhumiwa
wanavyoandaliwa mpaka kuanzia siku mbili kabla mpaka dakika ya mwisho ya
kuchinjwa… pia anaeleza kuhusu saikolojia na jinsi mtuhumiwa anavyokuwa
"desperate" dakika chache kabla hajachinjwa…
ADHABU YA KIFO HADHARANI NCHINI SAUDI ARABIA
Saudi Arabia ni moja kati ya nchi nne pekee ambazo bado zinatekeleza
adhabu ya kifo hadharani. Nchi nyingine ni Iran, Korea Kaskazini na
Somalia.
Nchini Saudi Arabia, serikali ya kifalme inatekeleza adhabu hii kwa msimamo kwamba wanatekeleza shari'ah kama ambavyo imeelekezwa katika Qur'an Tukufu.
Hivyo basi ikitokea raia amefanya kosa ambalo linapaswa aadhibiwe kifo,
adhabu hii inatekelezwa kwa mtu huyo kuchinjwa hadharani kwa upanga.
Makosa ambayo yanaweza kupelekea mtu kuhukumiwa kifo ni pamoja na Kuua,
usagaji, ushoga/ngono kinyume na maumbile, ubakaji, uzinzi, biashara ya
mihadarati, ukahaba, uasi wa dini au kisiasa, kuabudu sanamu, ujambazi
wa silaha, wizi wa kawaida (akiiba mara nne), kukufuru, uchawi na ulozi.
Japokuwa kumekuwa Ufalme wa Saudi Arabia umekuwa ukijitetea kuwa
wanatekeleza hilo kwa mujibu wa maagizo ya vitabu vitukufu, lakini watu
wengi wamekuwa wakitafsiri adhabu hizi za kuchinja watu hadharani kama
njia ya kujenga hofu mioyoni mwa wananchi ili waweze kutii kila jambo
ambalo linaamuliwa na mfalme wa Saudi Arabia na wasiweze kuhoji chochote.
Wajuzi zaidi wa elimu ya dini wanaweza kutujuza zaidi kuhusu hili, lakini binafsi kwa kadiri nilivyotafiti, nilichokiona kwamba
hukumu nyingi za watu nchini Saudi Arabia juu ya kuchinjwa hadharani,
japo zinatolewa kwa mtazamo wa kidini lakini zinaegemea zaidi katika
upande wa aina za hukumu za Tazir badala ya Hudud
Binafsi sina utaalamu sana kuhusu dini, lakini kwa "a, b, c" za dini
ninazofahamu, maoni yangu ni kwamba (nakaribisha kusahihishwa kama siko
sahihi) niseme natambua kwamba chini ya Shari'ah, kuna aina tatu za
hukumu. Tazir, Qisas na hudud.
Qisas ni aina ya hukumu ambazo zinakuwa baina ya pande mbili au mtu na mtu, yaani namna gani ya kumlipizia mtu aliyekutenda jambo fulani baya.
Kwa upande wa Hudud, hizi ni hukumu ambazo zimeonggelewa moja kwa moja
kwenye Qur'an. Yaani kwamba mtu akifanya kosa fulani basi adhabu yake ni
kifo hadharani. Hukumu hizi na makosa yake zimetajwa moja kwa moja
kwenye Qur'an na kwenye hadith.
Chini ya hukumu hizi, kuna angalizo/tahadhari kubwa inatolewa ili kuweza
kuepuka adhabu ya kifo hadharani pale inapobidi. Kwa mfano mtu
aliyehasi dini anaweza kupewa nafasi ya kutubu na kurejea tena kwenye
dini na kuondolewa adhabu ya kuuwawa hadharani.
Alafu pia kuna hukumu za Tazir. Hizi ni zile hukumu ambazo zimempa
mamlaka jaji wa mahakama (Kadhi) kutoa hukumu kwa utashi wake kutokana
na makosa husika kutotajwa moja kwa moja kwenye Shari'ah kwa mujibu wa
maandiko.
Sasa kwa maoni yangu, nchi ya Saudi Arabia wanatumia mwanya huu kushinikiza adhabu ya kifo hadharani ili kujenga hofu kwenye mioyo ya wananchi wake.
Jambo hili limekuwa linaleta shida sana kati ya Saudi Arabia na watu wa
haki za binadamu. Kuna makosa ambayo raia wa Saudi Arabia wanachinjwa
hadharani ambayo hata wanazuoni wengi wanaamini kwamba hayako sawa
kidini bali ni juhudi za Ufalme wa Saudia kuwaziba midomo raia 'vimbele mbele'.
Kwa mfano moja ya utata mkubwa kuhusu adhabu hii ya kifo hadharani ikitokea baada ya polisi wa Saudi Arabia kuwakamata vijana wawili walioitwa Ali al-Nimr na rafiki yake Dawoud al-Marhoon
kwa kosa la kuandamana mwaka 2011 kupinga utawala wa Kifalme nchini
Saudi Arabia. Kipindi vijana hawa wanakamatwa walikuwa na miaka 17
pekee.
Siku chache baadae alikamatwa muubiri wa kiislamu maarufu nchini humo kipenzi cha vijana anayeitwa Sheikh Nimr al-Nimr (mjomba wake Ali al-Nimr) kwa kosa la kutoa mawaidha yenye maudhui ya kupinga serikali.
Wote hawa walikatwa mwaka 20111 na 2012, na mpaka kufikia mwaka 2015
wote walikuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo kwa kuchinjwa hadharani.
Hukumu hii ili amsha hasira kubwa ya mashirika ya binadamu mpaka kufikia hatua utekelezaji wa adhabu kwa watuhumiwa hawa watatu ukasogezwa mbele, lakini bado wangali gerezani wakisubiria kuchinjwa siku yoyote ile.
(Sheikh Nimr al-Nimr walichinjwa mwaka jana, January 2, 2016 pamoja na raia wengine 47 kwa pamoja).
Lakini kila hii haimaanishi kwamba hakuna watu wanaochinjwa kila siku kwa amri ya serikali ya Saudi Arabia.
Tumezoea kuona vyombo vya habari vikiripoti kuhusu ukatili wa kikundi
cha ISIS kutokana na kuwachinja mateka wao wakiwa wanawarekodi, lakini
uhalisia ni kwamba serikali ya Saudi Arabia inachinja watu wengi zaidi
kuliko ISIS. Pengine habari za ukatili huu unaotekelezwa na serikali ya
Saudi Arabia haukemewi sana kwenye vyombo vya habari kutokana na
uswahiba wa serikali hiyo na mataifa ya kimagharibi yakiongozwa na
Marekani.
Mfano mwaka 2011 inakadiriwa kuwa watu 26 walichinjwa hadharani.
Mwaka 2013 zaidi ya watu 78 walichinjwa hadharani.
Mwaka 2015 jumla ya zaidi ya watu 158 walichinjwa hadharani.
Mwaka 2016 zaidi ya watu 153 walichinjwa hadharani, ambapo watu 47 kati
ya hao walichinjwa kwa pamoja (mass beheading) siku ya January 2, 2016.
UTEKELEZAJI WA HUKUMU YA KIFO KWA KUCHINJA HADHARANI
Kwa desturi siku ambayo hupendelewa kuchinja watu waliohukumiwa huwa ni siku ya Ijumaa asubuhi kabla ya jua kuwa kali au baada ya swala ya adhuhur.
Mwanzoni nilieleza namna ambavyo raia wengine wanaondolewa kwenye uwanja wa Deera Square ili kupisha zoezi hili.
Pia nimeeleza namna mtu huyu anavyoletwa mpaka hapa uwanjani aliwa amefungwa kitambaa cheusi na kupigishwa magoti.
Baada ya kupigishwa magoti, ndipo anaingiachinjaji ambaye mara nyingi atakuwa ni Muhammad al-Beshi akiwa na jambia lake kiunoni.
Kama mtu huyu anayechinjwa ni mwanamke, basi ni lazima aletwe hapa akiwa
amevalishwa hijab na akifika hapa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa
kumshika zaidi ya al-Beshi.
Lakini kama ni mwanaume basi unafuatwa tu utaratibu wa kawaida wa
kufunga kitambaa usoni (hata mwanamke naye lazima afungwe kitambaa).
Al-Beshi anaeleza kuwa katika kipindi hiki, mtu huyu anayetarajiwa
kuchinjwa anakuwa dahifu mno kisaikolojia kiasi kwamba karibia mara zote
huwa hawaletiushkeli wowote bali wanatij kila wanachoambiwa. Ni kana
kwamba wameshaitoa roho zao kwa mauti, yaani hawana tumaini tena.
Al-Beshi anaeleza kuwa mtu huyo anakuwa mnyonge katika kipindi hiki kiwango ambacho huwezi kushuhudia binadamu katika maisha ya kawaida.
Japokuwa anaeleza kuwa wapo wachache ambao huongea maneno ya huzuni na kulia kuomba huruma wasamehewe kitu ambacho (msamaha) hakijawahi kutokea.
Baada ya al-Beshi kuchomoa jambia lake kiunoni, anamsomea hukumu ya kosa alilolifanya huyo mtu na kisha kumkumbusha kutaja/kusoma "Shahada" huku awe anainamisha kichwa chake mbele akiwa hivyo hivyo amepiga magoti.
Kisha al-Beshi anainua jambia juu na kulishusha shingoni kwa mtu huyo
kwa nguvu, na kwa pigo moja tu anatenganisha kichwa na kiwili wili.
Al-Beshi akiwa anajiandaa kumkata mtu kichwa kwa jambia
Al-Beshi akiwa ameshamaliza kumkata mtu kichwa kwa jambia...
Ukitazama kwa makini hapo chini utaona mwili umelala ukiwa hauna kichwa
na kichwa kiko pembeni upande wa kushoto
Pigo hili moja la jambia linalotenganisha kichwa na kiwiliwili,
kinakitupa kichwa chini na kubiringika kama kichwa cha mdoli
kichodondoka chini huku kikiachwa mzoga wa mwili ukidondoka pembeni yake
ukibubujikwa na damu kutoka kwenye shingo ambayo haina kichwa tena.
Ndani ya kama dakika mbili hivi, wasaidizi wengine wanakuja na kuokota
mabaki ya mzoga huu wa binadamu na kuupakia kwenye gari inayosubiria
pembeni.
Sasa hapa inategemea na hukumu ya huyu marehemu ilivyoandikwa na Kadhi.
Kuna baadhi baada ya kuchinjwa hukumu yao inaamuru kuwa miili yao ininginizwe sehemu ya umma kwenye mti mrefu au 'crane' kwa siku tatu au nne au saba kutegemea na hukumu.
Lakini kama hukumu ya mtu huyu haisemi chochote kuhusu mwili wake
kuning'inizwa hadharani basi maiti hii inapelekwa mpaka mochwari ambapo
kichwa kinashonwa tena kwenye kiwiliwili kwa Uzi na sindano na kisha
mwili unazikwa.
Mpaka hapa hukumu ya kifo cha kuchinjwa hadharani inakuwa imekamilika.
Source: Jamii Forum
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
0 maoni :
Chapisha Maoni