DC LINDI AWATAKA WAZAZI KUSHIRIKI KATIKA KUWAWEZESHA VIJANA
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mkuu
wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga amewataka wazazi kuacha tabia
ya kuiachia Serikali na mashirika binafsi kuwawezesha vijana na badala
yake washiriki kuwasaidia vijana hao ili waweze kujitegemea.
Ameyasema
hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu nafasi ya
Serikali katika kusaidia maendeleo ya vijana waliomaliza mafunzo ya
ufundi chini ya Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa
na Shirika la Plan International.
Ndemanga
amesema kuwa mradi huo umeleta mabadiliko makubwa kwa vijana katika
eneo hilo kwani wamefundishwa sio tu mafunzo ya ufundi bali pia
ujasiriamali, namna ya kuweka hisa, kujiwekea fedha kwa ajili ya
matumizi ya baadaye pamoja na masuala ya kodi lakini tatizo
linalojitokeza ni wazazi kuwaachia Serikali na wadau wengine
kushughulikia kila kitu.
“Changamoto
ni nyingi katika kusaidia vijana hasa ambao tayari walishapata mafunzo
kwa sababu wazazi wakishafahamu kuwa vijana wao wako chini ya mradi basi
wanawaachia mzigo wote Serikali na wadau mbali mbali hivyo nawasihi
wazazi wawasaidie vijana wao katika kujitafutia ajira”.alisema Ndemanga.
Ametoa
rai kwa vijana kujitokeza kwa wakati pindi miradi hiyo inapotokea kwa
sababu wengi wao wamekuwa wakichelewesha kuleta maombi hayo mpaka muda
wa mafunzo unafika hivyo kwa kuwa mafunzo hayo hufanyika kwa muda
maalum, vijana wanatakiwa wajitokeze mapema kwa idadi kubwa.
Aidha,
Ndemanga amewataka vijana waliopata mafunzo kuwafundisha wenzao na pia
wanaojiajiri wakumbuke kuwaajiri vijana wengine ili kupunguza
mrundikano wa vijana wanaozagaa mitaani bila kuwa na kazi za halali.
Kwa
upande wake Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Hamida Mohamed amekabidhi
cherehani mbili kwa vijana wawili waliomaliza mafunzo ya ufundi chini ya
mradi huo ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha ushiriki wa wazazi
katika kuwakomboa vijana hasa kwenye masuala ya kiuchumi.
“Mradi
huu umetusaidia sana kuwaona vijana wenye mazingira magumu hasa
walemavu na kufahamu matatizo yao hivyo kutufanya sisi viongozi wa
Serikali kufahamu namna ya kuwasaidia huku tukisaidiana na wadau
mbalimbali”, alisema Mhe. Hamida.
Mradi
huo wa miaka mitatu 2015 hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa
mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya
Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya
ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
0 maoni :
Chapisha Maoni