BISHOP METHODIUS KILAINI |
BAADA ya mitandao ya kijamii pamoja na baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari kupotosha kuwa Kanisa Katoliki limemfungisha ndoa padri wake, imefafanuliwa kuwa, Padri akiomba kuondolewa upadri wake anaruhusiwa kuoa.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini ameeleza kuwa,katika wito wa Upadri katika Kanisa Katoliki , mapadri hawaoi na hiyo ni sheria ama nidhamu ya Kanisa siyo ya Mungu hivyo Papa ana uwezo wa kuitengua.
“Katika Kanisa Katoliki Padri ni kasisi, ni kuhani anayetolea sadaka altareni. Kutokana na nidhamu ya Kanisa Padri haruhusiwi kuoa lakini pale anaposhindwa kuendelea na wito wake ama anapoonekana kwamba anashindwa kuuishi upadri wake anaruhusiwa kuomba kuacha na anaruhusiwa kulingana na taratibu za Kanisa.
Mapadri ambao mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari vinazungumzia siyo mapadri walishafuata taratibu zote na kupata kibali kutoka kwa Baba Mtakatifu kuwa wamefunguliwa na upadri wao umeondolewa hivyo wana uhuru wa kuoa kwani wamefanywa walei si mapadri.
Padri akishavuliwa upadri haitwi tena Padri wala hawezi kutoa huduma kama padri, ana haki za kuishi ulei wake. Kulingana na taratibu za imani ya Kanisa Katoliki mlei anafunga ndoa aishi na mume ama mke wake kwa uhalali na kuweka maagano yao mbele ya Mungu na hapo hakuna kosa.
Tatizo ni tafsiri ya wanahabari kukuza mambo na kusema padri wa Kanisa Katoliki kaoa wakati alishaondolewa upadri.
Dr Wilbroad Slaa alikuwa Padri wetu tena Katibu Mkuu wa TEC ambaye nilimrithi lakini aliacha upadri kulingana na taratibu za Kanisa akaoa, huyu mwingine Kalugendo naye vilevile alifuata taratibu yupo huru na wako sahihi.
Hakuna aibu Kanisa Katoliki iliyopata wala halijakosea. Tuna taratibu zetu ni mambo tu ya kuelewa,” amesema Askofu Kilaini.
Kwa upande wake Padri Stefano Kaombe aliyefungisha ndoa hiyo katika Kanisa la Mtakatifu Petro Osterbay amesema kuwa, vyombo vya habari haviko sahihi kusema Padri wa Kanisa Katoliki ameoa kwani Kanisa likishamaliza taratibu zake za kumfanya padri mlei yaani kumuondolea ukasisi wake linamuondolea hadhi yake ya upadri.
“Kuna kuondolewa hadhi ya upadri na kufunguliwa kifungo cha useja. Mtu anaweza kufanywa mlei lakini kifungo cha useja kikabaki au unaweza kufunguliwa vyote.
Bw. Privatus Kalugendo alifunguliwa vyote Septemba 14 mwaka 2008 kwa hati ya Papa yenye Protokali No.4182/08.
Hivyo Bw. Kalugendo alikuwa huru tokea siku hiyo kufunga ndoa kwani hakuwa padri na hakufungwa useja.
0 maoni :
Chapisha Maoni