Waandishi wa habari wawili walioshiriki mbio za mwenge wa uhuru katika wilaya ya Singida, wamenusurika kufa baada ya gari aina ya Noah waliyokuwa wakisafiria kuacha barabara kisha kupinduka mara mbili.
Waandishi hao ni Elisante Mkumbo Mapicha (49) wa ITV na Redio One ambaye ameumia shingo na Doris Meghji (39) anayeripoti kituo cha runinga Azam TV mkoani hapa, yeye ameumia mkono wa kulia. Noah hiyo ilikuwa ikitoka kijiji cha Mtinko ikielekea Singida mjini.
Waandishi hao baada ya kumaliza mbio hizo juzi jioni, walilazimika kusafiri kwa Noah yenye namba za usajili T. 972 BPV, iliyokuwa ikiendeshwa na Bonifas Kibauri (25) mkazi wa kijiji cha Mtinko wilaya ya Singida.
Lengo lao lilikuwa kuwahi kutuma matukio yaliyojiri kwenye mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo. Waandishi wa habari hao walitibiwa katika hospitali ya mkoa mjini hapa na kuruhusiwa kurejea na majukumu mengine.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida,ACP Debora Magilingimba,akitoa taarifa juu ajali ya gari aina ya noah iliyojeruhi waandishi wa habari na abiria mwengine sita. (Picha na Nathaniel Limu)
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Julai, 2, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Debora Magilingimba, alisema ajali hiyo imetokea katika kijiji Mkenge kata ya Kijota tarafa ya Mtinko wilaya ya Singida saa 11.40 jioni.
Alisema Noah hiyo ambayo ilikuwa na abiria 11 na dereva pia imejeruhi abiria wengine ambao ni Ismail Abdalah mpiga picha mjini Singida, Neema Rashi (38), ameumia kichwani na Maria Emmanuel (7) wote wakazi wa mjini Singida, ameumia kichwa na mkono wa kushoto.
Alitaja wengine kuwa ni Ombeni Daudi (12) mwanafunzi Utemini sekondari ameumia kichwa na mkono wa kulia,Onesmo Daudi (16) mwanafunzi Senge sekondari ameumia mkono wa kushoto na Joice Daudi (14) mwanafunzi Utemini sekondari, ameumia kichwa na mkono wa kushoto. Wajeruhi walitibiwa katika hospital ya misioni Mtinko na kuruhusiwa.
“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali, ni uzembe wa dereva Kibauri ambaye alikuwa akilipita gari lililokuwa mbele yake, kwa kupita upande wa kushoto ambao sio wake. Pia alikuwa kwenye mwendo kasi kitendo kilichosababisha ashindwe kulimudu hilo gari,” alisema kamanda Magiligimba.
Aidha, alisema wamemtaka mmiliki wa noah hiyo,Khalifan Daniel Muro,kupeleka nyaraka za kumbukumbu za dereva wake aliyesababisha ajali hiyo. Dereva Kibauri, alifanikiwa kutoroka baada ya kusababisha ajali hiyo.
Mwandishi wa habari Ealisante Mkumbo, alisema walilazimika kusafiri kwa Noah hiyo baada ya kufanya juhudi kubwa kuomba gari kati yaliyokuwa yakitumika kwenye mbio za mwenge ili iwakimbize mjini Singida, kutuma matukio, lakini ziligonga mwamba.ws
“Nitumie fursa hii kuiomba serikali ya mkoa wa Singida,kutenga gari maalumu kwa ajili ya waandishi wa habari wakati wa mbio za mwenge wa uhuru. Huu mtindo wa kupewa gari ambalo lilikuwa linatumiwa pia na watu wa huduma ya afya, hauna tija kwetu. Kwa sababu endapo majeruhi watatokea, sisi waandishi wa habari, tutakosa gari,” alisema Mapicha.
Chanzo: Mo Dewji
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
0 maoni :
Chapisha Maoni