Aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora),
Sophia Simba,na pia Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), amekuwa akisemwa wakati mwingine kwa mafumbo kuhusu masuala ya mahusiano ya kimapenzi aliyopata kuwa nayo. Katika mahojiano na gazeti hili, mama huyo, miongoni mwa mambo mengine, aliamua kuwa muwazi juu ya mahusiano hayo na pia masuala kadhaa yanayohusu UWT.
Raia Mwema: Wasomaji wetu wangependa kukufahamu kwa sababu mengi yamekuwa yakisemwa na yakinong’onwa hususan kuhusu elimu yako; labda kwa vile hawaifahamu vizuri. Unaweza kutupa CV yako kwa kifupi?
Mama Sophia Simba: Asante kwa kunipa nafasi hii adimu. Nimefurahi kwamba umeweza kufika ofisini kwangu na kuweza kuongea na mimi. Nashukuru kwamba umeona upo umuhimu wa watu kunijua mimi Sophia ni nani hasa.
Ni kweli maneno mengi yamekuwa yakisemwa ambayo hayapendezi, lakini nitafanyaje? Kwa hiyo, kwa kifupi sana ningependa nikufahamishe labda pengine kwa kupitia wewe watu watanifahamu.
Mimi naitwa Sophia Simba. Ni Sophia Mathew Simba. Nyambi ni jina langu la nyumbani. Wazaramo wana majina yao ya ukoo, kwa hiyo mimi ni Nyambi na mdogo wangu alipewa jina lingine. Nilipokuwa mdogo baba yangu akasema huyu ni Nyambi.
Kwa kifupi sana, mimi ni mtoto wa mfanyabiashara. Baba yangu alitokea Kisarawe, kijiji kinachoitwa Sungwi. Baba yangu alisoma Minaki. Alipomaliza Minaki alirudi hapa Dar es salaam. Baba yangu aliwahi kufanya kazi mpaka ya uvuvi. Aliacha shule kutokana na umbali kutoka kijijini kwake Sungwi kwenda Minaki.
Watoto waliokuwa wakitoka bara walikuwa wanasoma boarding, lakini watoto wa Kisarawe wenyewe walikuwa wanatakiwa watembee umbali mrefu. Kwa hiyo, kutokana na hiyo alifikia mahali haikuwezekana.
Baba yangu mwanzoni alikuwa Mwislamu. Alikuwa anaitwa Omari Simba. Kutokana na kusoma pale Minaki, aliamua kubadilisha dini. Baba yangu alibatizwa katika Kanisa la St. Albans – hili la hapa mjini. Na baada ya hapo baba yangu aliondoka akaenda Morogoro kufanya shughuli za biashara.
Kule alikutana na mama yangu, mwanamke wa Kiluguru ambaye naye historia yake alikuwa Sister wa Roman Catholic. Kwa hiyo walikutana na wakaoana.
Katika maisha yetu yote tumeishi kama Wakristu wa Roman Catholic. Mpaka leo mimi ni Mroman Catholic ingawaje kila mtu ananipa dini ambayo anaitaka. Kwa hiyo, mimi ni mmoja wa watoto tisa. Mimi ni wa pili.
Raia Mwema: Makazi yenu hasa yalikuwa wapi?
Mama Sophia Simba: Makazi yetu yalikuwa Dar es salaam na Morogoro. Dar es Salaam tuliishi Bungoni, Ilala. Lakini tukiwa wadogo kabisa baba yangu alijenga nyumba yake ya kwanza kabisa Morogoro, Kwa Kingu.
Alifanikiwa sana kwa shughuli za baa. Mimi ni mtoto ambaye nimesomeshwa kwa pesa za pombe. Baba yangu alikuwa na baa inayoitwa Uzaramo Bar, Morogoro lakini pia alikuwa na baa inayoitwa Simba Bar. Kwa hiyo, mimi kufungua vizibo vya bia najua.
Nikiwa bado mdogo nilikuwa nauza mishikaki. Siku zote nyumba yetu ilikuwa upande baa, upande tunaishi sisi. Kwa hiyo, baba yangu aliendelea na shughuli za baa muda mrefu.
Raia Mwema: Ulianza shule wapi?
Mama Sophia Simba: Mimi nilianza shule Morogoro katika shule inayoitwa Kilakala, baada ya hapo nikapelekwa shule ya boarding inayoitwa Ilonga Middle School, Kilosa. Baada ya hapo nikasoma Forest Hill Secondary School. Sisi ndiyo waanzilishi wake.
Ule mwaka ambao wanafunzi wengi tuliambiwa hatukuchaguliwa tuliunganishwa darasa la saba na la nane. Kwa hiyo sisi tulimalizia darasa la nane. Huo ulikuwa mwaka 1965. Shule nyingi (za binafsi) zilianzishwa mwaka huo. Shule za Kibohehe, Forest Hill, Mzizima na Kinondoni, zote zilianza wakati huo.
Baada ya pale nikaenda Kibosho Secondary School. Kwa bahati mbaya baba akafariki, wakati huo nikiwa nafanya kazi NDC. Kabla hajafariki, baba alitaka sana nifanye shughuli za biashara, niendeleze biashara ya familia.
Baada ya kumaliza shule nilichaguliwa nikasomee ualimu lakini sikwenda, na badala yake nikapata kazi NDC. Hapo NDC nilianza kazi 1971 hadi mwaka 1979.
Baada ya hapo nikaingia Lonrho Group of Companies baada ya kuacha kazi NDC. Kutoka pale nikaanza kazi Metal Engineering Industries Development Association (MEIDA) ambayo ilianzishwa na Waswedish. Nikiwa hapo nikaamua kwenda kusoma. Nilianza mafunzo ya Certificate of law mwaka 1985. Nilipenda sana kusomea sheria.
Mwaka 1987 nilianza kusomea shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na nikahitimu mwaka 1992 au 1993. Kuna mwaka hapo katikati chuo kilifungwa kwa sababu ya kuwapo mgomo.
Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu nikarudi kufanya kazi Metal Industries; kwani wakati nasoma walikuwa wamenipatia likizo isiyokuwa na malipo. Baada ya kurudi walinipandisha cheo kuwa legal and administrative officer; kwani kabla ya kwenda chuo kikuu cheo changu kilikuwa administrative officer tu.
Wakati niko NDC nilikuwa katibu wa tawi la UWT la NDC na Mama Anna Mkapa alikuwa mwenyekiti wetu, tulifanya mambo mengi mazuri.
Chanzo: Raia Mwema
About Unknown
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 maoni :
Chapisha Maoni