Arsenal wazima mbio za Manchester United
Arsenal walifikisha
kikomo mkimbio wa Manchester United wa mechi 25 bila kushindwa kwa
kuwalaza mashetani hao wekundu 2-0 mechi ya Ligi Kuu ya England
Jumapili.
Ushindi huo uliweka hai matumaini ya Arsenal ya kumaliza
katika nafasi nne za kwanza, ingawa bado watatarajia timu nyingine
zijikwae.Mabao ya Arsenal yalifungwa na Granit Xhaka na Danny Welbeck kipindi cha pili.
Jose Mourinho aliwatuma uwanjani Marcus Rashford na Jesse Lingard kujaribu kuokoa timu yake lakini walishindwa kuwakomboa.
Matokeo hayo yamewaacha Arsenal wakiwa nafasi ya sita, alama mbili nyuma ya United ambao wanashikilia nafasi ya tano na sita nyuma ya Manchester City ambao wanashikilia nafasi ya nne.
Hata hivyo, Arsenal wana mechi moja ambayo hawajacheza.
Pamoja na kufufua matumaini ya Arsenal kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, ushindi huo wa Jumapili pia ulisaidia kufifisha rekodi mbaya ya Wenger dhidi ya Mourinho.
Katika mechi 15 zilizochezwa awali, Wenger hajawahi kuishinda timu iliyokuwa inanolewa na Mourinho, isipokuwa mchezo mmoja tu wakati wa mechi ya Ngao ya Jamii mwaka 2015.
Mourinho alikuwa ameshinda mechi nane, na hizo nyingine saba zikamalizika kwa sare.
Mourinho anaamini kushinda Europa Ligi ndiyo njia rahisi zaidi kwa United kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.
Baada ya kushinda dhidi ya Celta Vigo Alhamisi, United watarejea tena EPL kwa mechi dhidi ya Tottenham Jumapili tarehe 14 Mei.
Arsenal wana mechi ya katikati ya wiki ugenini Southampton Jumatano.
Chanzo: Swahili BBC
0 maoni :
Chapisha Maoni